Wednesday, February 22, 2012

Ruge, Sugu wamaliza tofauti

MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi na Mkurugenzi wa Clouds Media, Rugemalila Mutahaba jana walitangaza kumaliza tofauti zao zilizodumu kwa zaidi ya miaka miwili baada ya kufanyika kwa vikao vya usuluhishi.

Kikao cha mwisho cha upatanishi kilifanyika jana na kuratibiwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi pamoja na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.


Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Waziri Nchimbi ambaye alifuatana na Ruge na Sugu, alisema katika upatanishi huo pande zote mbili ziliridhika kuwa msingi wa mgogoro wao ni kila upande kuwa na kundi la wasanii na kuamini upande mmoja hautendei haki upande mwingine.


Alisema pande hizo mbili pia ziliridhika kwamba mgogoro huo baina yao badala ya kuimarisha upatikanaji wa haki za wasanii unadhoofisha jitihada hizo.


“Pande hizo ziliridhika pia kuwa mgogoro baina yao unajenga uhasama na utengano mkubwa miongoni mwa wasanii ambao wanapaswa kuungana kudai na kusimamia maslahi yao, hivyo Mbilinyi na Mutahaba wamekubaliana mambo manne,” alisema Waziri Nchimbi.


Aliyataja makubaliano hayo kuwa ni pamoja na kumaliza mgogoro na uhasama baina yao kuanzia jana, watashirikiana kufanikisha haki na jitihada ya kuinua maslahi ya wasanii na kuwaomba watu wote wanaowaunga mkono wamalize uhasama na kufungua ukurasa mpya na ushirikiano baina yao.


Pia alisema Mbilinyi na Mutahaba wamekubaliana kufanya jitihada ya pamoja ya kuunganisha vyama vya wasanii vya Tuma na TFU ili kutetea maslahi ya wasanii wakiwa na umoja zaidi.


Kwa upande wake, Mbilinyi alikiri kuwepo kwa vita ya muda mrefu baina yao ambapo alisema anaamini vita yenye malengo mwisho wake lazima ifikie suluhu kama walivyofanya wao.


Naye Mutahaba alishukuru hatua waliyofikia na kusema kuwa inawezekana walivyokuwa wakivutana nayo yanazidi kudhoofisha tasnia ya wasanii hivyo wameamua kuachana nayo na kusonga mbele kutetea haki za wasanii.


Hata hivyo alisema atahakikisha nyimbo za wasanii zinapigwa katika vyombo vyake kwa usawa ili kuhakikisha mianya kama uonevu na rushwa havina nafasi.

No comments: